JIPENDE

Jipende, jisheue, jilee, jienue, jifurahishe. Hakuna atakayekufanyia hayo zaidi ya wewe mwenyewe.

-FaFI

WAJA

Wapo waja wasiobebeka ni wazito kisha wanateleza. Wengi wasioridhika wana tamaa kisha ni wateuzi. Wachache walio waaminifu na watakao kukubali kwa kila hali yako. Usijenge chuki kwa yeyote kwani chuki ni mmea wenye sumu ya kuuwa uhusiano. Kuwa mwingi wa kusamehe na mwepesi wa kuridhia.
Muhimu, usimfanyie mtu jambo lolote ukitarajia malipo kwake. Tenda kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.

 

VIJIKUMBO

Unani na vijikumbo , jamani wangu mpenzi,

Yafahamu haya mambo, hayataki paparazi,

Ya pupa ni ya kitambo, nielewe laazizi,

Jitunzie chako chombo,kwa mapenzi na henezi ,

Sipapie kombokombo, makinika na ulezi,

Si yoyote mwenye fimbo, ni hodari kirumbizi.

~ Fatma Shafii

USHIRIKINA

“Kueni, ndipo mutakapogundua kuwa ushirikina upo ndani ya majumba yetu!” haya ni maneno katu siwezi kuyasahau ambayo niliambiwa na swahiba wangu.
Kwa hakika hayakuwa maneno yake bali ni maneno walioambiwa na mjomba wao wakiwa wao ni wangali wadogo.
Ni jambo la kusikitisha mno kuona kuwa asilimia kubwa ya watu ni washirikina.
_

Mitihani ya maisha tumeumbiwa sisi wanaadamu. Huenda jambo likakufikia na ukashindwa na namna zote za kupata suluhu. Hakika, ni wakati mgumu sana na pengine huchangia mtu kukaribia kukata tamaa, au kupata mafadhaiko . Naamini suluhisho pekee ni kumwelekea MwenyeziMungu kwani anasema kwenye kitabu chake tukufu, “…Naitikia maombi ya mwombaji anapo niomba. Basi na waniitikie Mimi, na waniamini Mimi, ili wapate kuongoka.” (Surah Al- Baqara – 186)
_

MwenyeziMungu ndiye aliyetuumba. Yeye pekee ndiye anayetujuwa kwa kila kitu. Matakwa na shida zetu anazifahamu vizuri. Lililo heri na lisiloheri nasi pia anatambua vyema sana.
Ni wajibu wetu, tufikwapo na mitihani ya kimaisha tumwelekee yeye na tuwe na subira. Katu tusiwe na fikra ya kutafuta suluhisho kwa namna zisizofaa na zenye kuleta maangamizi. Hatimaye, inatulazimu kukubali matokeo ya jambo lolote na tumshukuru MwenyeziMungu. Mwisho wa siku, alilolikadiria yeye ndilo huwa.
_

Hakika ya muumini siku zote akifikwa na jambo zuri hushukuru kwasababu ni heri kwake, na jambo baya likimtokea husubiri, kwani nalo pia ni heri kwake.

 ~ Fatma Shafii