UMEWAHI KUPANDA FERI?

Hivi umewahi kupanda feri?  Feri ni chombo cha kusafiria majini kinachotumiwa kuvusha watu, magari, pikipiki, mikokoteni, baiskeli na mizigo kutoka ng’ambo moja ya mathalan mto hadi nyingine. Feri ni nyenzo muhimu katika kuzalisha maendeleo. Vilevile, ni Johari adimu na adhimu. Pasingekuwapo na feri mambo tumbu nzima yasingeweza kufana.

 

Kama mkaazi wa Mombasa nchini Kenya, ningependa kuongea kuhusu feri yetu ya Likoni. Hakika, feri zilianza kufanya kazi mnamo mwaka wa 1937. Mv mvita na Mv Pwani ndizo mojawapo za feri za kwanza kufanya kazi. Kila baada ya mda fulani shirika la KFS (Kenya Ferry Services) wamekuwa wakileta feri aula kushinda za hapo awali.

 

Gharadhi au azma yangu ya kuandika ujumbe huu sio kukupa historia ya feri bali ni kukueleza kwa fusuli ewe mpenzi msomaji mambo utakayo kumbana nao ukiwa unalekea kwenye kivuko chetu cha Likoni hapa Mombasa.

 

Kwanza kabisa, utashangaa na kusangaa kuona halaiki ya watu wanaoteremka kuelekea kivukoni. Ni wengi mno. Utadhani ni waja wametolewa mji hivyo wanahujuru kuenda mji mwengine. Wazee kwa vijana, wake kwa waume, wazima kwa walemavu, wanene kwa wembamba. Kila mmoja yumbioni aidha kuelekea kupanda feri au wametoka kushuka sasa wanaelekea mjini kwa shughuli zao. Asilimia kubwa ya umma huo huwa  wako harakani. Ni kama wamechelewa sehemu wanayoenda. Hakuna mwenye utulivu. Iwapo utatokea kuenda na umezubaazubaa huenda ukapigwa vikumbo kila wakati. Kando na watu, kuna biashara zilizoanikwa pande zote mbili za barabara. Wachuuzi nao wamejaa. Almuradi, ni sehemu ilo changamfu sana.

 

Baada ya hapo, mna geti la kiingilio kwa wanao elekea kuvuka. Ndani yake kuna mashini za kuchunguza bidhaa walizobeba abiria pamoja na abiria wenyewe. Ambapo ukishapita hapo ndipo utakapoelekea kwenye sehemu ya kusubiri feri iwasili. Sehemu hiyo imegawanywa mara mbili, ipo sehemu moja hususan ya vilema, wanawake wenye watoto na mizigo alafu ipo ilobaki ya jumuia yote.

 

Kawaida, utakaribishwa na sauti halwa ya marimba. Marimba ni ala ya mziki mfano wa sanduku hutengenezwa kwa mbao na vibao vyembamba hutandikwa. Vipigwapo virungu viwili hutoa sauti. Marimba hiyo sanasana huchezeshwa na mtu asiyeona yaani kipofu. Mcheza marimba huyo huburudisha watu na kuziliwaza fikra nyingi ziliopo kwenye vichwa vya watu pamoja na kusairi hari tele lilojaa humo na  machovu ya watu walionayo baada ya kufanya kazi kutwa nzima. Iwapo utahisi uburudisho huo umekugusa na zaidi uwe na mkono uso mkongwe basi ungemtilia pondo mzee huyo kwa kumwekea japo senti fulani kwenye sanduku hilo.

 

Mwia mwingine, unaeza wakuta wanamaiyoga wenye umri mdogo sana wakisaka riziki kwa kuwatumbuiza abiria kabla kuabiri feri. Aidha, upo wakati huweko mchekeshaji anayetumbuiza waja kutumia maneno. Mchekeshaji huyu huwa kachambua maisha kila upande. Si upande wa siasa, si upande wa hali ya uchumi na kadhalika. Angelikuchekesha kwa nususi ambazo asaa kwa siku zako za kawaida usingeliwahi kufikiria au kuzingatia mambo hayo.

 

Licha ya hayo, masikio yako yangeshtuka kutokana na sauti ya juu ya mhubiri. Sauti hiyo ingewaamsha wafu kutoka kwenye makaburi yao masahaulifu. Mara nyingi huhubiri bila kipaza sauti. Husema kama upatu ungedhani hamezi mate.  Mhubiri farisi huyu angalikunasibisha kwa idili na kani almuradi umsikize. Angelinena neno la bwana hadi asiye na shughuli naye likamfika japo moja au mawili ya bibilia. Kulingana na hali uliyo nayo mda huo, mauburi hayo yangekuwa ima kama burudisho, kielemisho au hata kama kero tu ikiwa umechoka kupindukia. Jamani, mgala muue, ila haki yake mpe. Mhubiri huyo huyo hukuonya haswa uchunge mizigo yako kabla haijapata mmiliki mwengine.

 

Yupo ‘Mswahili msema kweli’. Rijali mmoja asiye kikongwe wala kijana. Iwapo mawazo yamekuzonga, ghafula huzuka ghulamu huyu atakayeiba ‘attention‘  yako yote kutokana na maneno yake matamu kama asali ya malkia nyuki. Sanasana huvaa kanzu na huwa na kigunia ambacho hukiangata mgongoni. Huyu bwana sijui kameza kamusi au vipi? Au pengine kahifadhi kitabu cha Felix Ochieng kiitwacho Stadi za Uandishi. Mdomo wake umejaa ndarire za ukweli na zilo kadhibu. Yapo yenye natija na yapo ya kuburudisha tu. Huenda akaanza ghafla kwa kusema,

“Niseme ama nisiseme?” na baada ya kujibiwa aseme,  basi huanza kusimulia hadithi,

“Hapo zamani za kale, palikuwa na…”

Walakin, haikuwa hadithi tu ya kawaida, sana angetoa hadithi yenye maudhui yalinganayo na haja zake. Angelitoa hadithi ya fulani aliyependa kuauni au kusaidia wenzake. Almuhim akutie fahamu nawe unyoshe mkono umpe naye japo ghawazi akali kwa hiari na mukhitari wako.

 

Hewala! Sio tu masikio yatakayokuwa yakishughulishwa hapo, hadi macho. Kando na kutazama mazingira, macho huhusishwa kilazima na matangazo ya biashara kwani maozi hayana pazia. Kuta zimejaa karatasi zenye matangazo kila aina. Kwa mfano, mna matangazo ya kazi ambazo ukweli kuhusu kazi hizo siufahamu. Kuna matangazo ya viwanja viuzwavyo, na shule zinazoibuka wanazoamini kuwa ni shule faridi. Bila kusahau matangazo ya waganga. Waganga wanaojivisha koja la udaktari kwa kutanguliza majina yao kutumia neno la daktari Fulani. Waganga wanaojiamini kutibu yalo maradhi na yasiyo maradhi. Kulingana na matangazo hayo wanatibu mambo kama mapenzi, biashara, kinga boma, kesi, kazi na nguvu za kiume. Yapo pia matangazo ya suluhisho ya wanaume wenye shida za kazi za kitandani. Ebo! Nisiseme mengi, ukitaka kujua zaidi kuhusiana na hilo nenda ukavuke feri.

 

Ikirari, sauti ambayo huwezi kosa kuisikia ni sauti za sarafu. Hii ni kawaida kama sharia. Sarafu zinazorushwa kwenye mikebe. Mikebe hiyo hubebwa na watu wenye ulemavu hususan vipofu. Hutembea katikati ya adinasi na kurusha mikebe hiyo kuashiria kuomba msaada wa fedha kutoka kwa wa waabiri. Wakati mwingine mikebe hubebwa na insi asiye mlemavu. Mzima kama kigongo walakin ubavuni, amemshikilia kipofu anamtembeza huku akimsaidia kuomba. Jambo hili hunipa mawazo tata, hivi mtu mzima yule hakuweza kutumia nguvu zake kufanya walau kibarua na kumsaidia mlemavu yule? Kuliko kumrangisha mlemavu kuanzia anga liwapo na uchechea hadi lifinikwe na utusi. Chambilecho wenye ndimi za uhenga, “Duniani kuna vituko na vitushi”.

 

Alhasili, sio kila insiya huburidika na matendo ya watumbuizi hao. Hivyobasi, shirika la KFS, wamewaekea runinga abiria. Wanatazama huku wakisubiria feri ifike. Ila sidhani kama runinga hiyo huwashwa mda wote. Juu ya yote hayo, wapo ambao watakuwa ‘busy’ kwenye rununu zao mda wote . Pengine wameshazoea hadi kuyaona mambo ya kawaida au wana shughuli muhimu wanafanya kwenye simu zao. Au utapata watu wanapiga soga tu.

 

Atafutaye hachoki, na akichoka keshapata. Wachuuzi kwenye sehemu hii hawakuachwa nyuma. Sifa moja kubwa kuhusu bidhaa wanazo uza inasemekana kuwa za rahisi sana. Jambo sijalichunguza ni ubora wa bidhaa hizo. Tende kwa shilingi kumi kumi, ‘pampers‘ kwa shilingi kumi na tano na mengineyo mengi kwa bei ya ubwete. Yupo muuzaji mayai stadi sana. Yaani amebobea kwa kiasi cha kwamba angelikuchambulia yai na akuwekee na kachumbari kwa sekunde zisizozidi ishirini. Pengine uhodari huo unatokana na hasara anayopata pindi anapomchambulia mtu yai alafu feri inawasili ghafla kuwafanya wateja wake kukimbilia forodhani wakimwacha na mayai yake.

 

Labek! Muacha mila ni mtumwa. Miaka nenda miaka rudi. Ulimwengu umekuwa ukiendelea kwa kasi ki upande wa teknolojia. Walakin, wapo wapigaji picha wa kutumia kamera. Hawa huwakosi. Husimama ufuoni wakiwasubiri watalii ili waweze kuwapiga picha kwenye mazingira yaliyo na feri katika bahari.

 

Jamani! Kuna masinzia. Unawafahamu hawa? Wamejaa mno. Tuseme hatujui wako kwenye hali gani. Hali ya ubinadamu, ama upepo. Ungalisahau kibeti chako wazi kibahati mbaya basi ungalifika ng’ambo ya pili kibeti hakina chochote. Wakati mwingine wanaiba hata kama vibeti vimefungwa. Hutawaona wakiiba, hutawasikia wakiiba ila utakuja kugundua tu washaiba. Ni mashetani watu.

 

Feri inapowasili na mageti kufunguliwa, ndipo umati wa watu unapoanza kubanana na kusukumana ilimradi kila mmoja anataka kuingia feri wa kwanza. Wanatawanyika nje ya geti hilo kama kuku watokao kibandani. Wanatoka nduki hadi kwenye feri hiyo. Hata wakaonywa mara ngapi kuwa watembee taratibu hakuna asikizaye. Jambo zuri ni kuwa mageti hayo hufunguliwa baada ya magari, pikipiki ,malori na mabaiskeli kuingia feri.

 

Feri hupakia kila kitu. Tena vitu vizito mno. Maumbile yana shani. Mathalan, chombo kizito kuelea majini, ilhali kitu chepesi kama sindano huzama, hakilei. Waamba huamba, utashangaa ferry .Jihadi zako zakuwania nafasi zitakapoisha utapigwa na kipepo kizuri cha bahari. Bahari kubwa iliyotanda na iliyo tulivu na tuvu. Bahari iliyonyooka twaa usione hata inapoishia. Kuntu, Mungu ni mwenye uweza wa kila jambo.  Hapo ndipo utatia ukitoa, uwaze ukiwazua bila dhiki wala kero lolote. Kuko makini sana. Wakaa mwingine, waeza kubahatika kuona meli kubwa zinapita. Meli za kila nui zinazotoka nchi tofautitofauti. Mandhari hayo yanakutuliza na kuhisi ni kama unaliwazwa na maumbile ya MwenyeziMungu. Upo wakati huwepo mawimbi makubwa hivyobasi kutetemesha feri kwa kiasi kidogo tu na kusababisha mititigo. Kama ulikuwa umeshasikia ajali chache za feri basi uta ‘panic’ kwelikweli. safari yenyewe ni kama takriban dakika ishirini hadi kufika ng’ambo ya pili.

 

Ufikapo ng’ambo ya pili, Likoni, utaona njia zilizoenuka juu mathalan milima. Ipo sehemu ya magari, na sehemu iliyo na ngazi ambapo abiria hupanda. Upande huu hutakaribishwa na marimba wala viburudushi vyovyote, bali wachuuzi na matingo au mataniboi ndio watakao kuwa wenyeji wako. Mtu wa kwanza utakaye pambana naye ni mzee anayeuuza dawa ya kunguni. Yeye husimama juu ya ngazi hizo akiwakasubiri abiria. Hunadi dawa zake aziuzazo kwa bidi sana. Hata kama hakuna kunguni mastakimuni mwako, wazo la kununua dawa hiyo lingekupita japo mara moja. Juu ya forodha hiyo utapata magari ya kuenda sehemu tofauti ya kusini mwa Pwani. Sehemu kama Ukunda, Kwale, Msambweni, Shimoni, Lungalunga na kadhalika. Zipo pia pikipiki za kuwapeleka watu waendao eneo zisio za mbali. Halaiki hiyo ya watu hutawanyika na kila mmoja kuelekea anakokwenda. Hivyo ndivyo hali ilivyo kivuko cha Feri Likoni mjini Mombasa, bukrata wa ashiya.

-FaFi