MAPENZI AU HELA

Hamujambo waungwana, natumai muwazima
Nimekuja kwenu tena, nina jambo la kusema
Limenitatiza sana, nimeshindwa pa kupima
Kwenye mapenzi na hela, lipi nd’o chaguo jema?

Akimpata Kijana, an’empenda mazima
Mapenzi kila aina, mwanamume kujituma
Akamganda kwa sana, yupo na yeye daima
Kwenye mapenzi na hela, lipi nd’o chaguo jema?

Lakini huyu Kijana, mifuko ina tetema
Mingwenje inahepana, hana hata za kupima
Kila siku yeye hana, na kutupa malawama
Kwenye mapenzi na hela, lipi nd’o chaguo jema?

Akimpata Katana, mwenye hela nyingi jama,
Hamfanyii khiyana, masilahi kutimiza
Ngwenje anazitawanya, mithili anavyohema
Kwenye mapenzi na hela, lipi nd’o chaguo jema?

Katana mahaba hana, kubembeleza kakwama
Jambo la kutetezana, halimo katika kima
Na kwenye kuridhishana, hayupo huko kahama,
Kwenye mapenzi na hela, lipi nd’o chaguo jema?

Fikirieni kwa kina, kisha nd’o muje kusema
Nionyesheni baina, pale pa kupatazama
Ni Kijana au Katana, amfaaye Halima?
Kwenye mapenzi na hela, lipi nd’o chaguo jema?

SIKU TATANISHI

Siku zimebadilika,
Nyumbani
Nyumbani sio nyumbani tena
Kuta zimegeuka
Ghafula zinachomeka
zinawaka kuwaka
Paa linapeperuka
limeteketea
limechoka kustahamili
linakwenda juu kwa juu
Hewa nayo inafuka moto
ndipo kukawa na jingi joto
Milango na madirisha
Yamegeuka
yamekuwa kuni zinazozidisha
Moto utokao kwenye kuta

Ndugu amebadilika
Haijui thamani yangu
Haijui thamani ya mwanangu
Haijui thamani ya mama
Sote anatumaliza

Kila kuchapo
Mwana kaibiwa
Amekula kichapo
Na viungo kutolewa

Wamezuka majini watu,
Mahayawani watu
Waso haya na utu.

Roho zimegutuka
Hakuketiki, hakulaliki
Hapakaliki ila kwa roho juu juu
Nyumbani sio nyumbani tena
Dunia imebadilika
Nyumba sasa ni kaburi
Linatumeza tukiwa hai.

SARAFU YA KORONA

Bila shaka, janga la Covid-19 limekuwa jambo la kawaida na sivyo kuogopewa kama pale awali. Corona ni familia ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa mafua, homa na kuendelea kuwa kali inaposababisha matatizo ya kupumua. Ni mripuko uliogunduliwa mwaka wa 2019.

Ujio wa Corona umebadilisha mambo mengi katika maisha yetu. Kwa mfano, namna tunavyosalimiana na pia tunavyojumuika na wenzetu hadharani. Janga hili limewaathiri waja pakubwa sana, hususan vijana. Kwanza kabisa, kuja kwa Corona kulisababisha wasiwasi kwa namna unavyosambaa haraka na kuua. Kwasababu hii, serikali ililazimika kufunga vyuo ili kuokoa maisha ya vijana. Ikafikia kufunga mipaka ya miji iliyoathirika sana na kampuni nyingi kufungwa. Hatua hii ilichangia ukosefu wa ajira kwa vijana katika sekta mbalimbali. Hali zikawa ngumu. Ukosefu wa ajira kwa njia moja au nyengine imesababisha ongezeko la uhalifu mitaani.

Alhasili, kampuni nyingi zimepunguza watu kwaajili ya Corona walakin sio wote wanaokosa ajira huingia kwenye uhalifu. Wapo wenye nidhamu ambao hutafuta mbinu aula za halali. Kuna wale wanaokosa kabisa kukidhi hata mahitaji ya kimsingi na ndipo dhiki zinapowasonga. Huzuni na hatimaye kupata unyogovu. Unyogovu pia huwezwa kusababishwa na upweke wa kukosa kutangamana na wenzao. Hali hii humaliza nguvu katika utendakazi na pia fikra zao. Unyogovu hueza kufanya kijana akajiua. Baadhi wanaojipata hapa hukata tamaa na kutokea kuingia kwenye mihadharati. Mihadharati hunyonya afya zao, huzipoteza ndoto zao, huziua aila zao na kusababisha uhalifu kuzidi.

Waambi huamba, mgala muue na haki mpe. Minghairi ya maafa maovu mna mazuri pia yanayotokana na janga hili. Naam, wako vijana wanaofaidi kwenye ajira kama vile biashara za barakoa na vieuzi. Mna ajira zilizotolewa na idhara ya afya ikiwa ni njia mojawapo katika mikakati ya kupambana na Corona. Ukosefu wa kazi, kumewafanya vijana kuzingatia kazi za mkono na za ubunifu kama vile kuandika. Hii imeboresha ujuzi wa vijana.

Ikhilasi, usafi umedumishwa. Tumekuwa tukiosha mikono yetu kila mara kwa kutumia vitakasa. Makaazi, mitaa na majumba yamekuwa yakisafishwa mara kwa mara ili kuviua virusi hivi. Isitoshe, kipindi hichi cha Corona, kumekuwa na ongezeko kubwa kwa vijana katika utumiaji wa teknolojia. Mikutano, warsha, mafunzo na kadhalika zinafanywa mitandaoni. Hii imerahisisha mambo mengi pamoja na kuepuka uwezekano wa kupata maradhi haya.

Hatimaye, naweza kusema kuwa janga hili ni kama msumeno, hukata mbele na nyuma. Tukumbuke kuwa maisha yanapokuwa jasiri inatulazimu tujasirike. Inatupasa kumuweka MwenyeziMungu mbele na kumuomba atuepushe na maradhi haya. Nasi vijana tunafaa kushirikiana, kuelimishana na kusaidiana, katika kipindi hichi cha janga la Corona, ikirari, nguzo moja hiajengi nyumba.

VIJARUNGA NA MITANDAO YA KIJAMII

Samahani kijana, tafadhali iweke simujanja kando. Sio lazima uchapishe mtandaoni namna daktari anavyokudunga sindano. Nakuomba, uiweke rununu kipembeni, haina haja kuonyesha waja msaada unaopeana.

Samahani kijana, jaribu kutembea bila kutazama simu japo kwa mda tu, badala yake angalia watu na mazingira. Isitoshe, ukiwa kwenye shughuli zenye watu, jifundishe kuweka simu kando na kutangamana na wenzako. Tena, sioni umuhimu wa kuweka mtandaoni unapoabudu. Unatuomba sisi au MwenyeziMungu?

Samahani vijarunga, leo ningependa kuingilia maisha yenu. Nataka niwaulize munaoweka kila jambo la maisha yenu mitandaoni munashindana na nani?

Faragha katika maisha kwa kiasi fulani ni muhimu sana. Ni kipi tunachokitafuta haswaa katika mitandao? Umaarufu? Tazama jinsi jamii inavyopelekwa mbio na mitandao hii. Vipaumbele katika maisha na nia za kutenda mambo hivi sasa imebadilika.

Shinikizo rika na kutojithamini ni sababu miongoni mwa sababu zinasosababisha mtu kuchapisha maisha yake mitandaoni. Sababu hizi humfanya mtu kuona anahitaji upendekezo fulani kutoka kwa watu, hivyobasi anatupa mambo tumbunzima. Wengi wao huweka mambo mazuri tu. Kwa mfano, wataeka picha ya sehemu za starehe walizoenda, picha za vitu vizuri wanazo miliki au zisizokuwa zao. Wataongea kuhusu kila jambo litakalowapa ‘attention’ watakaposambaza kwenye mitandao. Mambo haya huwafanya kujiona kuwa na thamani, kwa namna wanavyopokelewa mtandaoni. Tatizo ni kuwa matokeo yake ni kushindwa kujidhibiti. Kushindwa kuijua mipaka ya yanayopendekeza na yasiyopendekeza kuwekwa. Wanakataa kufikiria wanachokiweka kitaleta faida au hasara katika maisha yao na wenzao.

Yakini, munajidanganya kwa kudhani mitandao ya kijamii inawapa thamani kutokamana na upande mmoja wa uzuri munaoonyesha. Thamani ni jambo linalotokana na mtu binafsi. Ni pale mtu anapotambua hadhi na heshima yake. Shida ni kuwa, hatutambui kujithamini bora ni kule kukua bila ya kuogopa kutofaulu kwani kutofaulu hakubadilishi wala hakuharibu hadhi ya mtu.

Jambo la kusikitisha, utaona vijana wakifanya mambo pasi na uwezo wao.
Wanang’ang’ana vilivyo, ima kwa njia za sawa au zisizo sawa ilimradi aweke mtandaoni kama wenzake. Ni heri ikiwa tutaachana na vitu vinavyopita uwezo wetu. Hamu ya kutaka kuishi maisha tusiyoyaweza ni mbaya. Iwapo tumekosa uwezo wa kumiliki kitu, afadhali
tukiwache na ikitokea kuwa ni lazima kukipata basi aula tukifanyie kazi.

Je, nitakosea nikisema utumiaji wa mitandao ni kama utumiaji wa sigara? Hakika, sioni tofauti kwani tushakuwa waraibu. Imefika kuwa hatuezi kuenda bila simu. Tukiibiwa simu tunanyauka, tunajawa na huzuni na tunakosa utulivu wa roho. Kama vile tunavyoweza
kufanya mambo mengi tukitumia simu zetu basi halkadhalika tusipokuwa nazo.

Samahani kijana, naomba ukimaliza kusoma ujumbe huu, iweke simu kando na utafakari niliyokuambia.

KAZI YA KUTAFUTA KAZI

Najua ni muda mrefu sana tangu mwisho kuandika . Nimekuwa nikipigana na fikra zangu juu ya kuandika suala hili. Moyo mmoja ukiniambia nisiliandike huenda nikajiharibia na mwengine ukinihimiza niliandike huenda nikawatia moyo wenzangu tulioko kwenye jahazi moja. Na sasa naliandika ila bado niko katika njia panda ya kuendelea au kuwacha.


Sio rahisi kwa mtu kufungua roho yake na kusema jambo linalomkera kwa mwia mrefu. Katu sio rahisi kumwaya yanayonichoma mtima kila kukicha. Pengine inaweza kuwa ni kutokana na matumaini mengi nilioyaweka hapo awali au tuseme ni ukosefu wa kuwa na subira ya hali ya juu. Subira nilionayo imenifikisha hapa baada ya kungoja kwa miaka minne na bado naendelea kusubiri.
Labda nikuulize tu mwenzangu, hivi umekaa mda gani tangu umalize chuo kikuu bila ya kupata kazi? Tupo wengi au nipo pekeyangu? Tangu nilipohitimu shahada yangu mwaka wa 2016 hadi wakati huu ninaoandika ujumbe huu, sijafanikiwa kupata kazi. Nashukuru niliweza kufanya industrial attachments kwa kampuni chache. Safari hii kamwe haijakuwa rahisi. Upo wakati ilinifisha moyo sana kufikia hata kujuta kusoma walakin minghairi ya hisia hizo, ugumu wa maisha hunilazimu kuendelea kutafuta kazi hadi dakika hii. Kwa hakika, nahisi kama Kenya ina wenyewe, na ndio maana niliwahi kuweka maoni yangu kwa machungu wakati nilipoona ndugu yetu katibu wa baraza la mawaziri, Mheshimiwa Bi. Nadiya Ahmed, kaweka mtandaoni kuwa “Kenya ni mimi na wewe”. Hapana, haiwezekani. Kenya hii naishi kwa imani tu. Maonevu na mapendeleo niliyokuwa nikiyaona hainipi haki ya kusema Kenya ni yangu. Wale wanaopata wakitakacho kwa njia zisizo za sahihi bila kuchukuliwa hatua yeyote. Wale wenye mali tumbu nzima na makampuni na wamesalia kuandikana wao kwa wao. Hao ndio wenye nchi. Sisi walalahoi, tusiokuwa na jamaa zetu waliopo kwenye nyanja za juu. Sisi tuliofundishwa na wazazi kwa shida na hali za kifukara na kufikia kumaliza akiba yao yote, mbona tupotupo tu tukitumiwa kama vijego vya kuwaenua wengine.
Wacha leo nikupe historia fupi ya safari yangu ya ku tarmac. Pindi tu nilipomaliza chuo kikuu, nilijawa na matumaini kuwa ningepata kazi nzuri kwa muda usiokuwa mrefu. Niliamini fika kuwa isingewezekana Mombasa hii ati ningekaa mwaka bila kupata kazi. Kumbe yalikuwa mawazo tasa. Sijakaa mwaka tu bali nimekaa miaka. Polepole nilianza kutafuta kazi. Nilianza na zile kampuni za ndoto yangu. Kampuni kubwa kubwa. Ukapita mda fulani hivi, bila majibu yoyote. Nikaamua kutafuta hata kwenye vijikampuni vidogo vidogo nikijiambia kuwa nitashikilia kiasi cha kupata kazi nzuri. Wapi? Wiki, miezi na hatimaye mwaka. Nikaona mambo hayakuwa kama nilivyotarajia, hivyo basi niliweka ratiba ya kutembelea kampuni kila siku nikiomba kazi. Uzuri nilisomea kuhusu fedha, kwahiyo niliweza kuulizia kazi katika kampuni yoyote. Nikaanza na kampuni zilizohusika na masala ya fedha. Wiki ya pili, nilikwenda kwenye mahospitali, wiki ya tatu katika kampuni za redio na kadhalika. Nilichapisha karatasi zangu na kuwa na nakala nyingi. Nilikuwa nikienda sehemu najieleza alafu nabwaga karatasi zangu. Nikaendelea vivyo hivyo kwa kiasi cha miezi miwili au mitatu sikumbuki vizuri . Hatimaye, niliamua kuenda mtaa ulioko na viwanja (godowns) mbalimbali, uitwao Labour hapa Mombasa. Nilianza mguu mosi mguu pili, kiwanja baada ya kiwanja kuanzia kiwanja cha kwanza hadi cha mwisho kutokea kufikia mtaa mwengine sehemu za Makupa. Yaumu hiyo katu siwezi kuisahau wala kuizika katika kaburi la sahau, maana nilirudi nyumbani viatu vikiwa vimetoboka.
Siku na miezi ikasonga, hamna lolote. Waah, nikaamua kuchukua hatua nyengine. Nikawa naenda mjini, nasoma magari, tisheti za watu walovaa, pikipiki, saa kubwa za barabarani zinazofadhiliwa na kampuni tofauti tofauti. Nilitazama kila kitu chenye jina la kampuni, nikiandika jina hilo kwenye simu. Alafu niliporudi jioni, nilikuwa nikizitafiti kwenye mtandao, zengine nikituma baruapepe na kutuma ombi langu la kazi, na zengine nikienda mwenyewe kwenye kampuni na kuwaeleza ombi langu. Jamani, kimya! Sikuvunjika moyo. Nilichukua hatua nyengine, nilienda kutoa nakala makaratasi yangu na kuingia kwenye magorofa marefu ya ofisi hapa Mombasa. Nilianza na jumba TSS, jumba la NSSF alafu jumba la Ambalala na kadhalika. Zipo afisi hazikuniruhusu hata kuingia ndani, hapa nilihitajika kumwachia askari gongo stakabadhi zangu.
Licha ya hayo, kuna wakati serikali hutangaza kazi. Ningezichangamkia haraka sana, juu ya gharama zilizoandamana nazo ikiwemo kutuma cheti cha Good conduct, cha HELB, cha EACC na kadhalika. Alafu sasa ubaya wa vyeti hivi vina expire baada ya mwaka. Kwa hiyo nimekuwa nikitoa mpya kila mwaka. Kuna sehemu zengine nilikuwa nikituma ombi langu la kazi mpaka nikaona ni kama kumpigia mbuzi gitaa. Ukija kusikiasikia vile watu hupata taabu baada ya kununua hizo nafasi kwa mapesa mengi. Pesa zenye hata sijawahi kuzifikiria, ingenifisha moyo sana. Hapo ndio ninashangaa sisi walalahoi nafasi yetu iko wapi? Mbona watangaze kazi, watutie hasara na kwenye madeni ya kutafuta stakabadhi hizo ilhali wanaowaandika tayari wanawajua. Ndipo nikasema, uchumi wa Kenya ni ule wa maskini kuzidi kuwa maskini na tajiri kuzidi kutajirika. Nimepeleka makaratasi yangu kwa kampuni zisizopungua mia tano. Hii Kenya ingekuwa yangu pia basi nami ningekuwa nipo sehemu flani na kazi inayoniwezesha kutimiza japo haja zangu muhimu za maisha.
Upo wakati hata najuta kwanini nilisoma. Mda wote niliotumia kusoma kwa shida na pesa tumbi nzima zilizoenda shuleni, hivi ningepewa tu pale nilipomaliza sekondari nikajifungulia biashara naona ningekuwa mbali sana. Laiti walimu wa vyuoni wangetutayarisha kisaikolojia kuwa kuna na kukaa miaka bila kazi kama vile walivyotutia hamu ya kuwa tungepata kazi haraka sana, pengine mambo yasingekuwa magumu kwetu kama yalivyo sasa. Kumbe kusoma haikuwa kazi bali kutafuta kazi ndio kazi. Nimedanganywa na watu sana kuhusu kupata kazi. Nimepuuzwa sehemu nyingi sana ninazoomba kazi. Wanachokitaka wenye kampuni sijui ni kipi ambacho mimi sina. Mara ooo you’re over qualified, mara ooo haujafikisha kiwango flani cha CPA, visababu vya kila aina vya kututoa njiani. Kilichowazidi wenye kazi sijui ni kipi kilichopungua kwangu. MwenyeziMungu anajua zaidi. Enyi matajiri, munatunyima kazi mukiwapa watu wenu ni sawa, ila kumbukeni huenda kesho nasi tukawa hapo tukitakiwa kuwaajiri watoto wenu. Ya Mungu ni mengi.
Matangazo yenyewe ya kazi ni ya kufisha moyo. Wanaeka kuwa wanahitaji mtu mwenye ujuzi wa miaka kadhaa. Sasa sisi wengine tuliotoka vyuo vikuu mda usio mwingi tutaajiriwa na nani? Kwanini musitupe nafasi angalau mukatuonyesha kazi ndio nasi tuwe sawa? Mwisho wa siku tunasalia kubaki majumbani miaka na miaka. Kukaa nyumbani tu haiwezekani tena, hali zimekuwa ngumu. Tunatokea kufanya kazi za kujitolea, ndio ati tujulikanwe na “wakubwa” ambao wanaeza kutupa kazi. Kazi tunajitolea lakini tunaumia, nauli ya kuenda sehemu hiyo kila siku tuitoe wapi? Chakula? Tunafanya tu kwasababu hatuna budi, lakini tunaumia sana. Walakin, sio wote wenye akili hiyo, wengine huwa wahalifu ili kutafuta riziki. Na wengine wakitafuta wa chumba waliowazidi umri, wenye hela zao, ili nao wapate tonge la siku.
Kutafuta kazi imekuwa kama kutafuta pepo. Kuna wakati natembea barabarani naona wanawake wenzangu wananipita na magari nashangaa kwani hawa walitumia njia gani? Mimi nilikosea wapi? Wanasiasa ndio hata usiseme. Ni warongo kupindukia. Hawana wanachofanya, kazi kutuahidi na kututia tamaa za kupooza. Zaidi, wanatutia na hasara kwa juu za kuwaandama kila siku maafisini na hawako. Nimekaa nyumbani mda mrefu imefikia kutumiwa kama mfano na jamaa zangu ambao wanao hawataki kusoma. Wakikanywa kuhusu watoto wao utawasikia, “Fatma huyo amesoma mpaka University amefika wapi? Kila siku yuko barabarani tu na makaratasi.” Aisee! Inauma. Inauma tena sana. Kalenda iliisha maana kwangu pindi nilipopata kofi la ufahamu wa uhalisia wa mambo. Jumatatu kwangu ni sawa na ijumaa na sawia na jumapili. Sioni tofauti ya tarehe moja na tarehe thelathini, mwanzo wala mwisho wa mwezi. Siku zangu zote ni sawa, niamke nitafute hiyo kazi, nihangaike kupata riziki, nirudi kulala jioni. Kuna wakati mashoga zangu niliosoma nao ambao walibahatika kupata kazi pamoja na jamaa, waliona heri wanitume kufanya shughuli zao town wakati wao wako busy makazini mwao alafu wanipe japo senti kidogo. Kikweli mimi ni mhitaji kwahivyo sikuweza kukataa, japo haikuwahi kuingia kwenye akili yangu kuwa ningefikia hapo. Nikasema haidhuru, muhimu nipate pesa au riziki ya halali. Nikawa naingia mjini nikiwanulia watu vitu na kuwatumia. Ikafikia siku moja mtu akaniambia, “Sasa siku hizi umekuwa hamali?” Nilihisi kanitia mkuki kwenye moyo wangu. Nilishindwa nimjibu nini, nilimezea huku machozi yakinilengalenga. Kutafuta kazi kumenifanya niwe depressed mara nyingi sana.
Unapokuwa huna kazi na umekaa nyumbani mda mrefu, watu wanaanza kukudharau. Hata wale ambao hawakusoma lakini wamejaaliwa kwa njia moja au nyengine kuwa na pesa, wanakukejeli. Marafiki wanafiki nao wanakuhepa. Wanakuona huna usaidizi wa aina yoyote. Wewe ndio utakayetumika kutimiza mambo ya wengine. Inauma lakini ndio ukweli. Binafsi nimeona maisha ni yenye pande mbili, masikini na matajiri, wazuri na waovu, wenye imani na wenye kukejeli na kadhalika. Mapema mwaka huu nilianza kusomea shahada mpya ya ualimu, baada ya kuahidiwa na mtu kuwa kampuni yao itanismamia kunifundisha. Ni jambo ambalo nililifikiria kwa mda mrefu sana. Nilihofu kufanya uzamili katika sekta ya fedha baada ya kuona shahada yake imenisumbua mno. Nikaona heri nibadilishe nijaribu kitu kipya. Kitu ambacho nakipenda sana. Haya basi, nikafanya nilichotarajiwa kufanya na hatimaye nikajiunga katika chuo kikuu cha Kenyatta University hapa jijini Mombasa. Nilisoma mwezi wa kwanza na wa pili ilhali bado sijalipa ada. Kumuuliza jamaa aliyeniahidi, aliniruka futi mia, simu nikimpigia hakushika kamwe. Nikajaribu mara kadhaa kila siku hakuwa akinishikia simu. Nikaamua kupigia simu kampuni iliyotarajiwa kunismamia moja kwa moja. Kuulizia, niliarifiwa kuwa waliacha kitambo kulipia watu ada za shule, na huyo jamaa kumbe kafutwa kazi. Kaniletea kilio mazishini.
Aidha, nilipoona upande mmoja umelemea ilinishuruti kutizama wa pili. Baada ya miaka ya kutafuta kazi bila mafanikio nikaamua kuangalia wazo la kufungua biashara. Nikajaribu kuangalia vipengo katika soko mbali mbali. Nashukuru nilipata mawazo si haba. Sasa kuja katika kuianza biashara yenyewe ndio nilikwama. Hakuna pesa. Kila umfuataye analia yeye njaa. Serikali wanatoa pesa kwa vijana, zinazowafikia wanaowataka wao. Kupata mfadhili wa biashara ikawa kama kupata kazi. Nikarudi palepale. Leo huyu anidanganye anataka kunisaidia nimfuate mpaka nijue kumbe kanitapeli, kesho mwengine naye azuke aniahidi kunisaidia nimfuate hadi mwishoe nigundue ana njama chafu. Mawazo yangu ya kufungua biashara yakasalia vitabuni.
Mara nyingi huwaza na kujiuliza, ama pengine riziki yangu iliandikwa nitaipata vyengine na sio kupitia kuajiriwa? Mwisho wa siku huambia wenzangu, maadamu juu yetu kuna paa yaani tumestirika kwenye majumba, tuwazima na afya yetu, tunapata cha kutia mdomoni basi tumshukuru MwenyeziMungu sana. Naamini ipo siku riziki zetu zitasimama. Ipo siku tutakuja kupata kazi au kuweza kufungua biashara zetu zitakazo nawiri. Siku yetu inakuja. Tuzidi kuwa na imani na kuvuta subira. Hakuna refu lisilokuwa na ncha. Tulipotoka ni mbali ila tunapoelekea ni karibu. Ewe mola wangu tujaalie na sisi kazi zenye heri nasi, zenye usahali na kazi zitakazo tukuza kiakili na kimali nasi tuje tuwasaidie wenziwetu, Ameen.

UMEWAHI KUPANDA FERI?

Hivi umewahi kupanda feri?  Feri ni chombo cha kusafiria majini kinachotumiwa kuvusha watu, magari, pikipiki, mikokoteni, baiskeli na mizigo kutoka ng’ambo moja ya mathalan mto hadi nyingine. Feri ni nyenzo muhimu katika kuzalisha maendeleo. Vilevile, ni Johari adimu na adhimu. Pasingekuwapo na feri mambo tumbu nzima yasingeweza kufana.

 

Kama mkaazi wa Mombasa nchini Kenya, ningependa kuongea kuhusu feri yetu ya Likoni. Hakika, feri zilianza kufanya kazi mnamo mwaka wa 1937. Mv mvita na Mv Pwani ndizo mojawapo za feri za kwanza kufanya kazi. Kila baada ya mda fulani shirika la KFS (Kenya Ferry Services) wamekuwa wakileta feri aula kushinda za hapo awali.

 

Gharadhi au azma yangu ya kuandika ujumbe huu sio kukupa historia ya feri bali ni kukueleza kwa fusuli ewe mpenzi msomaji mambo utakayo kumbana nao ukiwa unalekea kwenye kivuko chetu cha Likoni hapa Mombasa.

 

Kwanza kabisa, utashangaa na kusangaa kuona halaiki ya watu wanaoteremka kuelekea kivukoni. Ni wengi mno. Utadhani ni waja wametolewa mji hivyo wanahujuru kuenda mji mwengine. Wazee kwa vijana, wake kwa waume, wazima kwa walemavu, wanene kwa wembamba. Kila mmoja yumbioni aidha kuelekea kupanda feri au wametoka kushuka sasa wanaelekea mjini kwa shughuli zao. Asilimia kubwa ya umma huo huwa  wako harakani. Ni kama wamechelewa sehemu wanayoenda. Hakuna mwenye utulivu. Iwapo utatokea kuenda na umezubaazubaa huenda ukapigwa vikumbo kila wakati. Kando na watu, kuna biashara zilizoanikwa pande zote mbili za barabara. Wachuuzi nao wamejaa. Almuradi, ni sehemu ilo changamfu sana.

 

Baada ya hapo, mna geti la kiingilio kwa wanao elekea kuvuka. Ndani yake kuna mashini za kuchunguza bidhaa walizobeba abiria pamoja na abiria wenyewe. Ambapo ukishapita hapo ndipo utakapoelekea kwenye sehemu ya kusubiri feri iwasili. Sehemu hiyo imegawanywa mara mbili, ipo sehemu moja hususan ya vilema, wanawake wenye watoto na mizigo alafu ipo ilobaki ya jumuia yote.

 

Kawaida, utakaribishwa na sauti halwa ya marimba. Marimba ni ala ya mziki mfano wa sanduku hutengenezwa kwa mbao na vibao vyembamba hutandikwa. Vipigwapo virungu viwili hutoa sauti. Marimba hiyo sanasana huchezeshwa na mtu asiyeona yaani kipofu. Mcheza marimba huyo huburudisha watu na kuziliwaza fikra nyingi ziliopo kwenye vichwa vya watu pamoja na kusairi hari tele lilojaa humo na  machovu ya watu walionayo baada ya kufanya kazi kutwa nzima. Iwapo utahisi uburudisho huo umekugusa na zaidi uwe na mkono uso mkongwe basi ungemtilia pondo mzee huyo kwa kumwekea japo senti fulani kwenye sanduku hilo.

 

Mwia mwingine, unaeza wakuta wanamaiyoga wenye umri mdogo sana wakisaka riziki kwa kuwatumbuiza abiria kabla kuabiri feri. Aidha, upo wakati huweko mchekeshaji anayetumbuiza waja kutumia maneno. Mchekeshaji huyu huwa kachambua maisha kila upande. Si upande wa siasa, si upande wa hali ya uchumi na kadhalika. Angelikuchekesha kwa nususi ambazo asaa kwa siku zako za kawaida usingeliwahi kufikiria au kuzingatia mambo hayo.

 

Licha ya hayo, masikio yako yangeshtuka kutokana na sauti ya juu ya mhubiri. Sauti hiyo ingewaamsha wafu kutoka kwenye makaburi yao masahaulifu. Mara nyingi huhubiri bila kipaza sauti. Husema kama upatu ungedhani hamezi mate.  Mhubiri farisi huyu angalikunasibisha kwa idili na kani almuradi umsikize. Angelinena neno la bwana hadi asiye na shughuli naye likamfika japo moja au mawili ya bibilia. Kulingana na hali uliyo nayo mda huo, mauburi hayo yangekuwa ima kama burudisho, kielemisho au hata kama kero tu ikiwa umechoka kupindukia. Jamani, mgala muue, ila haki yake mpe. Mhubiri huyo huyo hukuonya haswa uchunge mizigo yako kabla haijapata mmiliki mwengine.

 

Yupo ‘Mswahili msema kweli’. Rijali mmoja asiye kikongwe wala kijana. Iwapo mawazo yamekuzonga, ghafula huzuka ghulamu huyu atakayeiba ‘attention‘  yako yote kutokana na maneno yake matamu kama asali ya malkia nyuki. Sanasana huvaa kanzu na huwa na kigunia ambacho hukiangata mgongoni. Huyu bwana sijui kameza kamusi au vipi? Au pengine kahifadhi kitabu cha Felix Ochieng kiitwacho Stadi za Uandishi. Mdomo wake umejaa ndarire za ukweli na zilo kadhibu. Yapo yenye natija na yapo ya kuburudisha tu. Huenda akaanza ghafla kwa kusema,

“Niseme ama nisiseme?” na baada ya kujibiwa aseme,  basi huanza kusimulia hadithi,

“Hapo zamani za kale, palikuwa na…”

Walakin, haikuwa hadithi tu ya kawaida, sana angetoa hadithi yenye maudhui yalinganayo na haja zake. Angelitoa hadithi ya fulani aliyependa kuauni au kusaidia wenzake. Almuhim akutie fahamu nawe unyoshe mkono umpe naye japo ghawazi akali kwa hiari na mukhitari wako.

 

Hewala! Sio tu masikio yatakayokuwa yakishughulishwa hapo, hadi macho. Kando na kutazama mazingira, macho huhusishwa kilazima na matangazo ya biashara kwani maozi hayana pazia. Kuta zimejaa karatasi zenye matangazo kila aina. Kwa mfano, mna matangazo ya kazi ambazo ukweli kuhusu kazi hizo siufahamu. Kuna matangazo ya viwanja viuzwavyo, na shule zinazoibuka wanazoamini kuwa ni shule faridi. Bila kusahau matangazo ya waganga. Waganga wanaojivisha koja la udaktari kwa kutanguliza majina yao kutumia neno la daktari Fulani. Waganga wanaojiamini kutibu yalo maradhi na yasiyo maradhi. Kulingana na matangazo hayo wanatibu mambo kama mapenzi, biashara, kinga boma, kesi, kazi na nguvu za kiume. Yapo pia matangazo ya suluhisho ya wanaume wenye shida za kazi za kitandani. Ebo! Nisiseme mengi, ukitaka kujua zaidi kuhusiana na hilo nenda ukavuke feri.

 

Ikirari, sauti ambayo huwezi kosa kuisikia ni sauti za sarafu. Hii ni kawaida kama sharia. Sarafu zinazorushwa kwenye mikebe. Mikebe hiyo hubebwa na watu wenye ulemavu hususan vipofu. Hutembea katikati ya adinasi na kurusha mikebe hiyo kuashiria kuomba msaada wa fedha kutoka kwa wa waabiri. Wakati mwingine mikebe hubebwa na insi asiye mlemavu. Mzima kama kigongo walakin ubavuni, amemshikilia kipofu anamtembeza huku akimsaidia kuomba. Jambo hili hunipa mawazo tata, hivi mtu mzima yule hakuweza kutumia nguvu zake kufanya walau kibarua na kumsaidia mlemavu yule? Kuliko kumrangisha mlemavu kuanzia anga liwapo na uchechea hadi lifinikwe na utusi. Chambilecho wenye ndimi za uhenga, “Duniani kuna vituko na vitushi”.

 

Alhasili, sio kila insiya huburidika na matendo ya watumbuizi hao. Hivyobasi, shirika la KFS, wamewaekea runinga abiria. Wanatazama huku wakisubiria feri ifike. Ila sidhani kama runinga hiyo huwashwa mda wote. Juu ya yote hayo, wapo ambao watakuwa ‘busy’ kwenye rununu zao mda wote . Pengine wameshazoea hadi kuyaona mambo ya kawaida au wana shughuli muhimu wanafanya kwenye simu zao. Au utapata watu wanapiga soga tu.

 

Atafutaye hachoki, na akichoka keshapata. Wachuuzi kwenye sehemu hii hawakuachwa nyuma. Sifa moja kubwa kuhusu bidhaa wanazo uza inasemekana kuwa za rahisi sana. Jambo sijalichunguza ni ubora wa bidhaa hizo. Tende kwa shilingi kumi kumi, ‘pampers‘ kwa shilingi kumi na tano na mengineyo mengi kwa bei ya ubwete. Yupo muuzaji mayai stadi sana. Yaani amebobea kwa kiasi cha kwamba angelikuchambulia yai na akuwekee na kachumbari kwa sekunde zisizozidi ishirini. Pengine uhodari huo unatokana na hasara anayopata pindi anapomchambulia mtu yai alafu feri inawasili ghafla kuwafanya wateja wake kukimbilia forodhani wakimwacha na mayai yake.

 

Labek! Muacha mila ni mtumwa. Miaka nenda miaka rudi. Ulimwengu umekuwa ukiendelea kwa kasi ki upande wa teknolojia. Walakin, wapo wapigaji picha wa kutumia kamera. Hawa huwakosi. Husimama ufuoni wakiwasubiri watalii ili waweze kuwapiga picha kwenye mazingira yaliyo na feri katika bahari.

 

Jamani! Kuna masinzia. Unawafahamu hawa? Wamejaa mno. Tuseme hatujui wako kwenye hali gani. Hali ya ubinadamu, ama upepo. Ungalisahau kibeti chako wazi kibahati mbaya basi ungalifika ng’ambo ya pili kibeti hakina chochote. Wakati mwingine wanaiba hata kama vibeti vimefungwa. Hutawaona wakiiba, hutawasikia wakiiba ila utakuja kugundua tu washaiba. Ni mashetani watu.

 

Feri inapowasili na mageti kufunguliwa, ndipo umati wa watu unapoanza kubanana na kusukumana ilimradi kila mmoja anataka kuingia feri wa kwanza. Wanatawanyika nje ya geti hilo kama kuku watokao kibandani. Wanatoka nduki hadi kwenye feri hiyo. Hata wakaonywa mara ngapi kuwa watembee taratibu hakuna asikizaye. Jambo zuri ni kuwa mageti hayo hufunguliwa baada ya magari, pikipiki ,malori na mabaiskeli kuingia feri.

 

Feri hupakia kila kitu. Tena vitu vizito mno. Maumbile yana shani. Mathalan, chombo kizito kuelea majini, ilhali kitu chepesi kama sindano huzama, hakilei. Waamba huamba, utashangaa ferry .Jihadi zako zakuwania nafasi zitakapoisha utapigwa na kipepo kizuri cha bahari. Bahari kubwa iliyotanda na iliyo tulivu na tuvu. Bahari iliyonyooka twaa usione hata inapoishia. Kuntu, Mungu ni mwenye uweza wa kila jambo.  Hapo ndipo utatia ukitoa, uwaze ukiwazua bila dhiki wala kero lolote. Kuko makini sana. Wakaa mwingine, waeza kubahatika kuona meli kubwa zinapita. Meli za kila nui zinazotoka nchi tofautitofauti. Mandhari hayo yanakutuliza na kuhisi ni kama unaliwazwa na maumbile ya MwenyeziMungu. Upo wakati huwepo mawimbi makubwa hivyobasi kutetemesha feri kwa kiasi kidogo tu na kusababisha mititigo. Kama ulikuwa umeshasikia ajali chache za feri basi uta ‘panic’ kwelikweli. safari yenyewe ni kama takriban dakika ishirini hadi kufika ng’ambo ya pili.

 

Ufikapo ng’ambo ya pili, Likoni, utaona njia zilizoenuka juu mathalan milima. Ipo sehemu ya magari, na sehemu iliyo na ngazi ambapo abiria hupanda. Upande huu hutakaribishwa na marimba wala viburudushi vyovyote, bali wachuuzi na matingo au mataniboi ndio watakao kuwa wenyeji wako. Mtu wa kwanza utakaye pambana naye ni mzee anayeuuza dawa ya kunguni. Yeye husimama juu ya ngazi hizo akiwakasubiri abiria. Hunadi dawa zake aziuzazo kwa bidi sana. Hata kama hakuna kunguni mastakimuni mwako, wazo la kununua dawa hiyo lingekupita japo mara moja. Juu ya forodha hiyo utapata magari ya kuenda sehemu tofauti ya kusini mwa Pwani. Sehemu kama Ukunda, Kwale, Msambweni, Shimoni, Lungalunga na kadhalika. Zipo pia pikipiki za kuwapeleka watu waendao eneo zisio za mbali. Halaiki hiyo ya watu hutawanyika na kila mmoja kuelekea anakokwenda. Hivyo ndivyo hali ilivyo kivuko cha Feri Likoni mjini Mombasa, bukrata wa ashiya.

-FaFi

 

URAIBU WA MITANDAO YA KIJAMII

Samahani kijana, naomba uieweke simujanja yako kando. Sio lazima uweke mtandaoni namna daktari anavyokudunga sindano.

Samahani kijana, naomba uweke rununu kIpembeni. Haina haja kuweka mtandaoni kuonyesha waja msaada unaopeana kwa watu.

Samahani kijana, kwa dakika chache tu nakuomba utembee bila kutazama simu yako. Chukua mda huo kuangalia watu, vitu, njia na kadhalika.

Samahani kijana, ukiwa kwenye shughuli ya mkusanyiko wa watu, jaribu japo mara moja kuweka simu kando na kutangamana na ndugu jamaa na marafiki. Kuna umuhimu na faida pia katika kufanya jambo hilo.

Samahani tena kidogo, sio lazima ukiwa unafanya ibada utuwekee video mtandaoni. Unatuomba sisi au MwenyeziMungu? Wakati mwingine tunajikosesha malipo ya kitu kwasababu za kutaka kuonekanwa tu.

Samahani vijarunga, leo ningependa kuingilia maisha yenu. Najua hayanihusu ila kuna mda inakera. Je, ni mimi pekeyangu au wewe pia umegundua kuwa imekuwa  ‘too much’? Nishaandika kuhusu hili na saa hii naandika tena na nitaandika tena na tena hadi nitakapohisi kuwa sauti yangu imewafikia wahusika. Nataka niwausie nyinyi. Ndio, nyinyi munaoweka kila jambo la maisha yenu katika mitandao. Nyinyi munaotuanikia Baraka za ukweli na za urongo kwenye mitandao. Ningependa munifahamishe munashindana na nani?

Faragha katika maisha kwa kiasi fulani ni muhimu sana. Ni kipi tunachokitafuta haswaa katika mitandao ya kijamii? Umaarufu? Au ni kitu gani chengine?. Nashindwa kuelewa. Tazama jinsi jamii inavyopelekwa mbio na mitandao hii. Vipaumbele katika maisha yetu hivi sasa vimebadilika. Nia za kutenda mambo pia zimebadilika.

Shinikizo rika, kutojithamini na unyogovu ni sababu kidogo tu miongoni mwa sababu nyingi zinasosababisha mtu kutuchapishia maisha yake mtandaoni. Sababu hizi humfanya mtu kuona anahitaji upendekezo fulani kutoka kwa watu hivyobasi anatupa mambo tumbunzima kwenye mtandao.  Naweza sema ni asilimia kubwa ya watumizi hawa, huweka mambo mazuri tu. Kwa mfano, wataeka picha ya siku walioenda sehemu za starehe, kama vile mikahawani na kadhalika. Wataweka picha za vitu vizuri tofauti wanazo miliki au zisizokuwa zao. Wataongea kuhusu tabia zao nzuri, matokeo ya maisha mazuri na kila jambo zuri au jambo litakalompa mtu ‘attention’ atakapotuma kwenye mtandao. Bila shaka mambo mazuri haya hutufanya tukajidhania au kujiona na thamani ya juu, kwa namna tutakavyopokelewa mtandaoni. Walakin, jambo aula Zaidi ni kuwa matokeo yake ni kushindwa kujidhibiti. Kushindwa kuijua mipaka ya yanayopendekezwa kuwekwa mitandaoni na yasiyopendekeza. Tunakataa kufikiria tunachokiweka kitaleta faida au hasara katika maisha yetu na ya wenzetu. Mwisho wa siku, jambo la muhimu kabisa ni uamuzi wako. Jinsi utakavyoamua kutumia mitandao ya kijamii ndivyo itakavyokuathiri.

Yakini, wacha niseme munajidanganya tu kwa kudhani mitandao ya kijamii inawapa hadhi na kujiona muko na thamani kutokamana na upande mmoja tu wa uzuri munaoonyesha mtandaoni. Thamani ni jambo linalotokana na mtu binafsi yeye mwenyewe. Ni pale mtu anapotambua hadhi na heshima yake mwenyewe. Cha muhimu ni kwamba hatutambui kuwa kujithamini bora ni kule kukua bila ya kuogopa kutofaulu kwani kutofaulu hakubadilishi wala hakuharibu hadhi ya mtu.

Jambo la kusikitisha zaidi utapata vijana wasiokuwa na uwezo wa kufanya mambo ya kifahari wawe na lazima wayafanye. Wanataka kufanya mambo pasi na uwezo wao kung’ana’ana vilivyo, ima kwa njia za sawa au zisizo za sawa ilimradi tu naye aweke mtandaoni kama wenzake. Hii ni hatari kubwa sana. Ni heri ikiwa tutaachana na vitu vinavyopita uwezo wetu. Hamu ya kutaka kuishi mitindo ya maisha tusioyaweza ni kubwa sana.. Narudia tena, iwapo tumekosa uwezo wa kupata au kumiliki kitu Fulani, tafadhali tukiwache, ikitokea kuwa ni lazima kukipata basi aula tuifanyie kazi ili tuipate.

Je, itakuwa nimekosea nikisema utumiaji wa mitandao ya kijamii ni kama utumiaji kwa sigara? Hakika, sioni tofauti kwani tushakuwa waraibu na imefikia mda sasa hatuezi kuenda bila simu. Tukitokea kuibiwa au kupokonywa simu tunanyauka, tunajawa na huzuni utasema tumefiliwa, tunakosa raha, tunakosa utulivu wa roho  na tunahisi ni kama tunaachwa nyuma wenzetu wanasongea. Kama vile tunavyoweza kufanya mambo mengi tukitumia simu zetu basi halkadhalika tusipokuwa nazo.

Samahani kijana, nakuomba utakapomaliza kusoma ujumbe huu weka simu kando utafakari.

 

 

 

MAHABA NI KITU GANI?…MAHABA KITU CHA SHANI

MAHABA NI KITU GANI?

Ninalo jambo moyoni, huniweka matatani
Kilipima akilini, sipati ufahamuni
Nalileta kwenu nyinyi, naliweka barazani
Enyi kina mwafulani, mahaba ni kitu gani?

Mahaba ni kitu gani, hivi leo nambiani
‘Lijitia mahabani, tangia hapo zamani
Kajiona taabani, sisikii na sioni
Enyi kina mwafulani, mahaba ni kitu gani?

Mahaba ni kitu gani, naomba nielezani
Lijipata mashakani, kwa kunitenda fulani
Nikajawa na huzuni, furaha ikawa duni
Enyi kina mwafulani, mahaba ni kitu gani?

Mahaba ni kitu gani, e’ nifafanulieni
Naona ni matesoni, sipati picha kamili
Na furaha siioni, ni wingi wa idhilali
Enyi kina mwafulani, mahaba ni kitu gani?

Mahaba ni kitu gani, waungwana ambani
Alipendwa Fikirini, na mumewe Sulemani
Hakuiona thamani, akaingia mitini
Enyi kina mwafulani, mahaba ni kitu gani?
Mahaba ni kitu gani, sasa nichambulieni
Kwanini huyu Jelani, daima kwa wagangani
Anataka binti Shani, amtie mkononi
Enyi kina mwafulani, mahaba ni kitu gani?

Mahaba ni kitu gani, mulobobea semeni
Watu wako taabuni, kuko tenge tahanani
Nipe maana ya ndani, nielewe kwa yakini
Enyi kina mwafulani, mahaba ni kitu gani?

~FaFi

MAHABA KITU CHA SHANI
Swali ulilouliza, kwa sote wa barazani
Dada Fafi nakujuza, hili lataka makini
Najaribu kueleza, ulitie fahamuni
Mahaba ni kuikuza, hisia ilo moyoni

Mahaba yake maana, leo nakuelezea
Ni hamu yakushibana, na mwenzi wako sikia
Huwa wafurahi sana, yeye kikukaribia
Hadi nguo kukubana, kwa raha kukuzidia

Mahaba msisimko, wa mwili na roho pia
Huhisi viungo vyako, tikitiki nakwambia
Yeye akiwa hayuko, upweke hukujalia
Kakujaa sikitiko, waweza hata kulia

Mahaba ni kuridhika, na tabia za fulani
Ukazidi kumtaka, husikii na huoni
Chake atachokitaka, wampa bila uneni
Yeye akifurahika, nawe huwa furahani

Mahaba yakishakuwa, moyoni yamemakini
Huwa huioni njia, ngakutia matesoni
Mangumi angakutia, na makonde mgongoni
Ndo wamuona Asiya, hatoki kwa Sulemani

Mahaba ni kukubali, kasoro alizonazo
Ukamuona jamali, hata akiwa muozo
Utapigana vikali, akiletewa mzozo
Kwake huwa huna hali, yeye ndio yako nguzo

Mahaba kujitolea, kumkubali vyovyote
Moyoni akishakaa, huna amri yoyote
Waganga tawaendea, umshike kivyovyote
Si wamuona Shuweya, amewamaliza wote

RUIYA SALIM
Maiya

 

 

Ningependa izame kwenye kichwa chako kuwa wewe ndiye mwenye umuhimu zaidi katika maisha yako. Hivyo basi ishi ukijitizama, na kufanya mambo yanayo kuridhisha, mambo yanayo kukuza wewe mwenyewe. Jifurahishe unapofaulu jambo. Jipe moyo unapokosa mafanikio. Wasaidie na uwafurahishe wenzako pale unapoweza ila tambua fika kuwa wewe ndio dereve wa gari la maisha yako. jiwezeshe kujitegemea kimawazo. Amini fikra zako. Hakuna atakayeishi maisha yako, watakuwepo nawe ila hawatapitia unayoyapitia. Mwisho wa siku, wewe ndiye mwenye umuhimu zaidi katika maisha yako. Raha jipe mwenyewe.

-FaFi